Uzinduzi Usio Kamili: Ulazima kwa ‘Startups’

Tunzaa
4 min readJul 12, 2021

--

Sasa ni wiki 3 zimepita tangu tumezindua aplikeshini yetu ya Android, na bado tuna msisimuko; inasisimua, na kuna mengi ya kufanya. Licha ya msisimko mkubwa unaokuja na kitu kipya, unakuja na mabadiliko mengi ndani ya muda mfupi na majukumu ambayo haukuyatarajia.

Shida ya kufanya uzinduzi, hasa kama startup, ni kwamba unataka kuhisi kwamba “Hii ndio yenyewe! tumekamilisha, sasa tuiweke sawa.”, wakati kihalisia, hapo ndipo unapoanza. Kutokana na uzoefu wetu kama Tunzaa, tulizindua bila mawazo ya “Tumekamilisha!” bali, “Je! Una uhakika unataka hii iende kwa watumiaji?”. Bado kulikuwa na mengi ya kurekebisha, kujaribu na kufanya iwe kamilifu.

Tulizindua na mapungufu mengi ambayo yalionekana hata kwa mtumiaji!

Unashangaa? Fikiria sura yangu pale Mwanzilishi wetu, Ng’winula Kingamkono, alipotaka aplikeshini izinduliwe wakati bado ipo katika hatua za mwanzo. Nakumbuka wakati huo, dhahiri kabisa nilikuwa na mawazo ya kutokuwa na uhakika na kuchanganyikiwa. Watu watakuwa na mtazamo gani, bado ilikuwa haijakamilika. Nikiangalia nyuma hivi sasa, ninafurahi tulifanya hivyo.

Ukamilifu ni kujichelewesha tu kunakojificha kwenye pambo, somo ninalojikumbusha mara kwa mara.

Tulifanya mengi zaidi wakati wa uzinduzi kuliko hapo awali, kwa sababu tulihisi kama tupo kwenye hatari zaidi kwa kuruhusu watumiaji kuanza kutumia aplikesheni na macho yakituangalia.

Kwa ufafanuzi wa kile Ng’winula aliniambia kulinishawishi,

“Kutakuwa na matatizo kila wakati, haiwezi kuwa kamili. Angalia Twitter, bado wanaongeza huduma na kurekebisha vitu na imekuwa sokoni kwa muda gani? Unadhani wangezindua ikiwa wangesubiri programu iwe kamilifu?“

Alikuwa sahihi.

Sasa, wakati tunaendelea kujaribu kuikamilisha, kasi yetu ilikuwa polepole sana na hitaji letu la kushinikiza kufanya mambo halikuwa katika kasi nzuri kama ilivyokuwa wakati wa uzinduzi. Kwa hakika ni msukumo tuliokuwa tunauhitaji.

Hakika haikuwa rahisi, lakini ninafurahi kuwa timu yetu ilikuwa inasaidia sana na ilijitoa kufikia mahali tulipo — bado sio mahali tunapotaka kuwa. Lakini tumepiga hatua kutoka pale tulipokuwa hapo awali.

Ninaamini katika nyakati hizi za mitandao ya kijamii na kuongezeka kwa aplikesheni nyingi, kufanikiwa au la, hutupatia mawazo haya ya kuwa na aplikesheni kamilifu. Inapozinduliwa, basi inapaswa kuonekana katika njia fulani, au tuseme, kampuni iwe na njia fulani, ili kujiunga na ligi kubwa za aplikesheni zingine zinazopatikana sokoni. Wazo la ukamilifu.

Tunachofanya sio kujifunza kutoka kwa aplikesheni zilizofanikiwa na jinsi zinavyokua!

Kwa maneno ya Mkurugenzi Mtendaji wa Airbnb, Brain Chesky,

“Ikiwa ulizindua na hakuna mtu aliyegundua, zindua tena. Tulizindua mara 3.“

Ukisoma kwenye historia ya Airbnb na ukuaji wao utajifunza kuwa walianzia kwenye njia tofauti na waliyo sasa, na jinsi walivyopaswa kubadilisha soko lao ili waweze kuongeza mapato na kukuza biashara yao. (mfano kuuza ‘cereal boxes’, ili wapate mapato na kutangaza biashara yao). Walikataliwa na wawekezaji, hata kwenye Y combinator, na walizindua zaidi ya mara moja. Lakini pamoja na hayo yote, hivi sasa wamekuwa kampuni ya mabilioni ya dola.

Unaweza kusoma zaidi juu ya hadithi yao hapa.

Maana yangu ni kwamba: tunaona tu biashara kubwa / waanzilishi waliofanikiwa wana nini hivi sasa na tunataka hivyo, bila kuelewa kuwa ukuaji ni mchakato, haufanyiki mara moja. Unatakiwa kupigwa makonde kabla ya kujua jinsi ya kuyakwepa, uzoefu ni kujifunza, sio kupitishwa.

Ikiwa lazima uzindue zaidi ya mara moja kufika mahali unapotaka kuwa, fanya hivyo. Ikiwa lazima uzindue kukiwa bado kuna mapungufu mengi, fanya hivyo.

Lakini kamwe usilenge ukamilifu, kwa sababu ukamilifu sio ukweli; unachofanya ni kukupunguza kasi na kuunda picha ya kufikirika akilini mwako. Weka malengo kwenye ukuaji, mabadiliko na kuwa bora.

Kitu kinachotusaidia kama Tunzaa, ni kuwa na lengo, lengo ambalo haliishi na linaongezeka kwa kasi, na kulifanyia kazi. Lengo letu ni “Je! Tunaongezaje mapato?” na kila siku tunajiuliza swali hili; kutusaidia utendaji wa kazi zetu za kila siku na vile vile kupangilia majukumu ili kukuza Tunzaa.

Pamoja na haya yote, bado ninaamini tuna safari ndefu na nzuri ya kwenda, na hii sio njia yoyote ya kusema tumefika hapo, lakini uzoefu huu ni jambo ambalo wengi wetu hapa Tunzaa hatutalisahau kamwe. Ni jiwe la msingi tulilolihitaji ili kuendelea na kushinikiza ukuaji wa Tunzaa.

Imeandikwa Na Maryam Baba — Customer Experience

Imetafsiriwa Na Bernard Mwakililo — Digital Marketing Manager

--

--

Tunzaa

Tunzaa is a fintech product that improves financial habits of everyday Africans through gamification with a marketplace for goods & services.